Kwa nini Nairobi ni Shamba la Mawe

Wakati unasikia mtu anaimba wimbo wa "Umetutoa Mbali" ni bora ujue anaamaanisha kile anaimba. Sasa katika harakati za kutafuta kazi baada ya kufuzu, rafiki yangu Oyonde aliangukia fursa ya tangazo la kazi kwenye mtandao ambapo alituma ombi la kazi bila kusita. Siku chache baadaye akapigiwa simu akialikwa kwa ajili ya mahojiano ya kazi.


Sasa mojawapo ya mahitaji ya yale mahojiano ilikuwa shilingi mia tano kwa ajili ya uchunguzi wa kiafya, simu nadhifu ama ukipenda smart phone, kipakatalishi au laptop na suruali fupi aina ya kinyasa. Isitoshe pesa hizo m,tu alisatahili aje nazo siku hiyo ya mahojiano na wala sio kuzituma kwa njia ya Mpesa kama vile walaghai wengine hutaka. Oyonde kama mtafutaji kazi yeyote hangeweza kuona chochote kisicho cha kawaida cha kushukiwa hapo kwa hivyo alibaki ajipongeza na kungojea siku hiyo kwa hamu na ghamu. 


Hatimaye siku hiyo ya mahojiano iliwadia na kijana wetu akawasili katika pahali alipoelekezwa mahojiano yangefanyikia. Mahali hapo palikuwa ni katika jengo fulani katika barabara ya Ojijo mtaa wa Westlands. Hapakuwepo mpangaji mwingine yeyote katika jengo hilo. Kwa hakika hata mapambo ya ndani ama ukipenda interior finishing hayakuwa yamefanywa.


Sasa kufika pale walikuwa watu thelathini wa kuhojiwa. Mahali pale wenye kazi walikuwa wamejaribu kupafanya paonekane kuwa afisi tarajiwa ama ukipenda upcoming office. Rafiki yangu Oyonde na wenzake wakaelezewa kwamba afisi zile ni mpya na walikuwa katika harakati za kupata fanicha pamoja na bidhaa zingine za pale afisini. Palikuwepo na zulia nzuri ajabu sakafuni na viti vichache vizuri pia. Hata mtoto wa watu asione tahadhari yoyote.


Mnamo saa nne hivi wakaitwa kwenye sehemu fulani maalumu ili mambo yaanze. Wakaelezewa kwamba wangeanza na mtihani wa kiafya kabla ya mahojiano yenyewe. Na kwa ajili ya matokeo bora walielezewa kwamba walihitajika wafanye mbio fupi fupi kabla damu itolewe. Sijui mbona watu huwa wanadanganywa peupe na wanakubali maana najua hata mtu hali mahututi na yule maiti hupimwa bila ya sarakasi kama hizi. Sasa wakapandishwa orofa ya juu ambayo ilikuwa imeandaliwa kwa ajili yao kufanya haya mazoezi ya kuchemsha damu.


Pale juu vijana watiifu wakaambiwa watoe nguo zao wavae vinyasa vyao maana kama unakumbuka kila mmoja wao alibeba kinyasa chake. Pia walionyeshwa mahali kwenye sakafu ya chini iliyo salama ili waweke bidhaa zao ndio wapande juu wafanye mazoezi. Sasa kila mtu na kinyasa, wengine ni boxer pekee na wengine na nguo zingine aina aina. Wakaambiwa waendelee na huko kukimbia ama ukipenda jogging wataitwa chini mmoja mmoja.


Punde si punde, sekunde zikawa dakika na dakika zikawa nusua saa. Ajabu! Dakika thelathini baadaye watu wametokwa na kijasho hakuna mtu alikuwa ameitwa chini kwa mtihani wa kiafya. Oyonde akasikia moyo unamwenda mbio sana akihisi hali ya hatari. Yeye na jamaa mwingine wakateremka chini ili wachunguze kilichokuwa kinaendelea pale. Masalale! Walipigwa na butwaa kupata chumba kile kitupu bila hata zulia au chochote isipokuwa tu kokoto. Kumbe ni sehemu jengo mahame na hata lilifaa kubomolewa. Hivi kumbe wakifanya mbio pale juu, huku chini vitu vyao: simu, tarakilishi na pesa kwenye mifuko vilikuwa vinasanywa!


Hebu wazia kikundi cha vijana thelathini kwenye barabara za Westalnda bila mashati , long'i au viatu wakielekea kituo cha polisi cha Parklands kupiga ripoti kuhusu kutapeliwa. Sarakasi bin vioja iliyotamba pale kituoni ni hadithi ya siku nyingine. Wale askari kwa OB walikuwa wanavunjika mbavu zao na kuangusha bunduki kwa vicheko wakisimuliwa yaliyotendeka. Jinsi Oyonde na wenzake walipata nguo za kuvaa na nauli ya kurudi nyumbani ni Mungu tu anajua.

Comments

Popular posts from this blog

What Tibim and Tialala stand for

Don’t be Easily Deceived by so-called Prophet David Owuor

Did you know that High Heeled Shoes are a Curse?